Wanafunzi wakivuka ziwa Nyasa kuelekea shule.
SASA ieleweke wazi kwamba hali si shwari kati ya Tanzania na Malawi. Pengine ni vizuri kujiuliza leo ni kwa nini mtafuruku uchukue nafasi kubwa leo. Kivipi Mtanzania wa kawaida, aoneshwe kama ni jambo lililokuja ghafla?
Kimsingi, mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi umekuwapo kwa zaidi ya nusu karne. Hivi sasa umechukua sura mpya baada ya nchi hiyo jirani kusema ndiyo inayomiliki sehemu yote ya ziwa hilo.
Pengine kauli hiyo peke yake, isingeleta shari. Alama ya hatari imetokana na kauli ya vitisho, iliyotoka Serikali ya Malawi kwamba itafanya kila linalowezekana, ikiwamo kutumia nguvu za kijeshi kuhakikisha ziwa hilo linabaki kwenye himaya yao.
Picha iliyopo ni kwamba Malawi wameshaona Watanzania ni wapole. Kwamba ni waoga wa kupitiliza, kwa hiyo wakiambiwa kuhusu nguvu ya kijeshi, watarudi nyuma. Sijui uthubutu huu wameupata wapi lakini ninachowaza ni kwamba viongozi wa Malawi, wanahisi sisi ni mazezeta.
Vile ambavyo madai yao yalivyo hayana msingi na hayakubaliki hata kidogo, ndivyo ambavyo ukitafakari wanachokitaka kiwe, huku wakitoa vitisho vya kupigana vita, unaweza kujiuliza kuhusu wigo wa uelewa wao. Ni rahisi kuamini ndugu zetu hao wana dosari za kiufahamu.
Kweli Ziwa Nyasa lote ni lao? Huo mpaka ni wa namna gani hasa, kiasi kwamba eti Mtanzania akikanyaga tu maji ya ziwa hilo, anakuwa yupo Malawi. Muda wa kutafuta maelewano hawataki, wanakimbilia kwenye vita. Malawi wanahitaji kuwaheshimu Watanzania. Ni ukweli ulio wazi kuwa hii siyo mara ya kwanza kwa Malawi kutoa madai hayo, lakini ni mara yake ya kwanza kutumia kauli yenye vitisho vya kiwango hicho kinachoashiria vita kati ya Tanzania na wao. Madai hayo yalitolewa kwa mara ya kwanza na Rais wa Kwanza wa nchi hiyo, Dk. Kamuzu Banda.
Madai hayohayo, yalirudiwa na wanasiasa mbalimbali, akiwemo mmoja wa viongozi wa vyama vya upinzani, Chakufya Chiana. Baadhi ya maswali yanayoulizwa ni haya yafuatayo;
Je, ni mambo yapi yameshindikana kutatuliwa katika mgogoro huo kwa muda wote huo wakati kuna vyombo vya kimataifa vyenye uwezo na mamlaka za kusuluhisha migogoro kama hiyo? Pili, ni upande upi ambao umeonekana kukwamisha mazungumzo hayo?
Kwa muda mrefu yamekuwapo mazungumzo kuhusu mgogoro wa mpaka huo, kupanuka kwa mgogoro huo hivi sasa kumechochewa na dalili za kuwapo kwa kiasi kikubwa cha gesi na mafuta katika ziwa hilo na hatua ya Malawi kuingia mkataba na kampuni ya Surestream Petroleum ya Uingereza.
Kampuni hiyo, tayari imeanza utafiti na utafutaji wa nishati hiyo, ikiwamo sehemu za eneo la Tanzania katika ziwa hilo. Kauli ya shari ya Serikali ya Malawi ilitokana na hatua ya Serikali ya Tanzania kuitaka serikali hiyo kusitisha shughuli hizo hadi suala la mpaka litakapopatiwa ufumbuzi.
Je, baadhi ya mambo kwenye mgogoro yamekuwa yakifanywa siri? Mbona sasa hali ya amani imehatarishwa hivi sasa? Ukweli ni kwamba Tanzania na Malawi, zimekuwa na uhusiano mzuri kiasi cha wananchi wa pande zote katika mpaka huo kutembeleana, kuoana, kufanya biashara na hata kupata huduma zote pasipo kujali uraia wao. Mtazamo wangu unanifikisha kwenye jawabu kwamba endapo wananchi wa pande zote mbili wangejua nani amekuwa kikwazo katika juhudi za kutatua mgogoro huo, wangeweka shinikizo kwa viongozi wa pande hizo mbili na hatimaye kupata suluhu ya mgogoro huo.
Kwa kuangalia sura ya undugu uliopo kati ya Watanzania na Wamalawi, kwa hakika vita haitakiwi. Lakini tunafanyaje ikiwa ndugu zetu hao wanataka mapambano? Je, vita ni utashi wao au Malawi inatumiwa ili kutia dosari historia yetu nzuri, kwamba ni kisiwa cha amani? Muda utaeleza. Watanzania hatutakiwi kuombea vita kwa sababu hiyo siyo sherehe. Kwamba watu watakutana ukumbini, kucheza muziki, kula kuku, bata, kunywa supu na aina nyingine ya maakuli. Tukumbuke Vita ya Kagera iliyomwondoa Nduli Iddi Amin.
Vita hiyo kama mfano hai kabla ya kuingia kwenye vita na Malawi, iliigharimu Tanzania maisha ya watu na kubwa zaidi ni mali. Tanzania ilipata hasara ya fedha za kigeni zaidi ya shilingi trilioni 5. Wananchi wa leo, waliokuwa na akili timamu kwa wakati huo, wanakumbuka madhara makubwa yaliyotokea.
Kama ni ushauri, basi napendekeza kwamba mgogoro huo wa mpaka kati yetu na Malawi umalizike kwa pande zote mbili kufikia maridhiano badala ya vita. Lakini kama hawataki je? Na kwa nini watangulize kauli ya kutaka vita? Kama si tamaa ya mafuta na gesi, basi wametumwa kuvuruga amani yetu.
Kwa upande mwingine, Malawi haiwezi kulaumiwa kwa sababu mgogoro huo ni pandikizi la ukoloni uliotokana na mkataba wa mwaka 1890 ambao ulielekeza kwamba sehemu yote ya ziwa hilo iwe upande wa Malawi. Hata hivyo, swali la kujiuliza ni hili; Je, viongozi wa Malawi, wao hawatumii akili?
Kweli Ziwa Nyasa lote ni lao na Tanzania haina eneo kabisa? Tanzania inayo haki ya kumiliki nusu ya eneo la ziwa hilo kutokana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sheria ya Bahari ya mwaka 1982 inayotaka nchi zinazogawana eneo la bahari au ziwa zigawane eneo hilo nusu kwa nusu.
Chanzo: GPL
Copyrights Tabitha Hudson 2012
0 comments:
Post a Comment