WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema posho kwa ajili ya wenyeviti wa vitongoji na vijiji ambao wataambatana na makarani wa sensa zipo palepale na kwamba hawana haja ya kuhofu juu ya malipo yao.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Jumapili, Agosti 26, 2012) mara baada ya kuhojiwa na maafisa wa sensa kijijini kwake Kibaoni, wilayani Mlele, mkoani Katavi.
Waziri Mkuu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Sensa amewasihi wenyeviti hao waendelee na kazi yao bila wasiwasi wowote kwani watalipwa. “Ni kweli malipo yao yamechelewa, ni suala la wikiendi tu kuingilia hapa kati, lakini napenda niwahakikishie kwamba stahili zao zipo, wao wachape kazi tu!” alisisitiza.
Alisema ameona kwenye taarifa za habari kupitia baadhi ya luninga wakidai kwamba wameachwa katika malipo ya kazi hiyo lakini akatumia fursa hiyo kuwahakikishia kwamba watalipwa. “Nimeona kwenye TV wanadai kuwa wameachwa, si kweli. Nawahakikishia wote kwamba wako katika hesabu yetu na wote watalipwa,” aliongeza.
Akizungumzia kuhusu zoezi zima la sensa ya makazi na watu, Waziri Mkuu Pinda aliwaomba Watanzania watambue kuwa zoezi hili lilianza tangu mwaka 2004 na lina gharama kubwa kwani mpaka sasa limegharimu zaidi ya sh. bilioni 140/-.
“Hili ni jambo linalopaswa kupewa nafasi kubwa na kila Mtanzania kwani lengo lake ni kuiwezesha Serikali kujua idadi ya watu tulionao, na itusaidie kupanga maendeleo yetu,” alisema.
“Serikali inao mpango wa miaka mitano, ifikapo mwaka kesho na mwaka kesho kutwa tutaweza kujua malengo yetu na kuweka mbinu za kuitekeleza mipango yetu... ,” alisema.
Alisema ukweli huo unabainishwa na maswali yaliyomo kwenye dodoso la sensa ambayo yanalenga kujua jinsi za watu, umri wao, shughuli zao za kiuchumi na kuwaweka katika makundi ili iwe rahisi kuwahudumia. “Tunaangalia jinsi za watu, rika zao, na hata makundi ya walemavu ili tuweze kubainisha mahitaji yao na kuwafikishia huduma kwa urahisi,” alisema.
Aliwasihi Watanzania ambao hawatahesabiwa leo kuwa wavumilivu kwani zoezi hilo litaendelea kwa muda wa siku saba. “Makarani wataendelea kutembelea kaya kwa siku saba zijazo, cha msingi mkuu wa kaya aandae taarifa za watu waliolala kwenye mji wake usiku wa tarehe 25 kuamkia tarehe 26 Agosti, mwaka huu. Aorodheshe majina yao, umri wao, elimu yao, jinsi zao na shughuli ambazo wanazifanya,” alifafanua.
Kuhusu watu wanaopinga sensa, Waziri Mkuu alisema anaunga mkono kauli zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein la kuwataka Watanzania wote washiriki zoezi la sensa.
“Viongozi wetu wa kitaifa wamelielezea vizuri suala hili na hasa kuhusu kipengele cha dini. Hayo madai si zoezi lake kwa sasa,” alisema.
Copyrights Tabitha Hudson 2012
0 comments:
Post a Comment