Kajala Masanja (pichani kushoto) na kulia akitoka mahakamani |
SHAHIDI wa nne Monika Timber (41), amedai mahakamani katika kesi ya kula njama, kuhamisha umiliki wa nyumba na utakatishaji wa fedha inayomkabili msanii wa filamu nchini Kajala Masanja na mume wake Faraja Chambo kuwa nyumba hiyo ya washtakiwa iliuzwa wakati zuio lililotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) bado muda wake haujamalizika.
Kadhalika, shahidi huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kunduchi Salasala, amedai kuwa Takukuru walitoa zuio la nyumba hiyo kufanyiwa chochote ikiwamo kuuzwa hadi uchunguzi wa kesi ya utakatishaji fedha haramu inayomkabili mshtakiwa Chambo utakapomalizika.
Timber alitoa ushahidi wake leo mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo anayesikiliza kesi hiyo.
Akiongozwa na Mwendesha Mashtaka Takukuru, Leonard Swai shahidi huyo alidai kuwa taasisi hiyo ilitoa zuio la kwanza Julai 15, mwaka 2009 ikimtaka mmiliki kutofanya kitu chochote ndani ya miezi 6 kwa kuwa inafanyiwa uchunguzi.
Alidai kuwa baada ya muda wa zuio lile kumalizika, Takukuru waliwasilisha zuio la pili Februari 18, mwaka 2010 lakini kabla muda wake kumalizika nyumba iliuzwa.
"Nyumba ile ilipouzwa ofisi yangu haikuhusishwa na muuzaji wala mnunuaji ...nilihojiwa na Takukuru baada ya ile nyumba kuuzwa nikawaeleza sikuwa na taarifa kwa sababu zuio bado lilikuwa halijamalizika muda wake," alidai Timber.
Katika kesi hiyo, Kajala na Chambo, wanakabiliwa na shtaka la kula njama ya kuhamisha umiliki wa nyumba iliyoko Kunduchi Salasala jijini Dar es Salaam kinyume na kifungu cha 34 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 wakijua ni kosa kwani tayari Mwanasheria Mkuu wa serikali alishazuia kuuzwa kwa nyumba hiyo.
Shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Aprili 14, mwaka 2010 washtakiwa hao walihamisha isivyo halali umiliki wa nyumba hiyo kwenda kwa Emiliana Rwegarura huku wakijua imepatikana kwa njia ya rushwa kinyume na kifungu cha 34(2)A(3) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.
Katika shtaka la tatu ilidaiwa kuwa siku na mahali hapo washitakiwa hao walitakatisha fedha huku wakijiua ni kinyume na sheria hiyo.
Washtakiwa walikana mashtaka yote kwa nyakati tofauti kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana kisheria. Washtakiwa wako mahabusu mpaka kesi itakapotolewa uamuzi.
Copyrights Tabitha Hudson 2012
0 comments:
Post a Comment