Meneja Matukio wa Ukumbi wa Dar Live, Abdallah Mrisho, akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu burudani itakayotolewa siku ya Idd Mosi. Wengine pichani ni Msanii Linah Sanga (wa kwanza kulia), Promota wa ndondi, Kaike Siraj (wa pili kulia), Mratibu wa Burudani Dar Live, Juma Mbizo (wa pili kushoto) na Bondia Maneno Oswald (wa kwanza kushoto).
Maneno Oswald 'Mtambo wa Gongo' akitoa tambo zake jinsi atakavyomchakaza mpinzani wake Rashid Matumla.
Mratibu wa Burudani Dar Live, Juma Mbizo akielezea jinsi walivyojipanga kwa burudani hiyo.Juma Kassim Nature akiahidi burudani ya aina yake siku hiyo.
Linah Sanga akiwaahidi mashabiki wake kufika kwa wingi Dar Live siku ya Idd Mosi kushuhudia makamuzi ya aina yake.
Na Mwandishi Wetu
MABONDIA wakongwe nchini, Rashid Matumla ‘Snake Man’ na Maneno Oswald ‘Mtambo wa Gongo’, watapigana pambano la kustaafishana siku ya Idd Mosi kwenye Ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakhem, Dar es Salaam.
Pambano hilo, linaitwa la kustaafishana kwa sababu, bondia mmoja atakayepigwa, atatakiwa kustaafu ngumi kutokana na makubaliano ya pambano hilo.
Meneja Matukio wa Ukumbi wa Dar Live, Abdallah Mrisho, alisema kwenye mkutano wa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kwamba Matumla na Maneno watapigana pambano la raundi 10, kisha litafuatiwa na mapambano mengine mawili na atakayepigwa atastaafu ngumi.
“Mabondia wenyewe ndiyo walitaka kuwe na pambano la aina hiyo, kwa hiyo mashabiki wao waje kwa wingi Siku ya Idd Mosi Dar Live ili wapate picha ni nani kati ya mabondia hao anaweza kustaafu,” alisema Mrisho na kuongeza:
“Siku hiyo itakuwa ni uzinduzi mpya wa Ukumbi wa Dar Live, kwa hiyo kutakuwa na shoo kali ya muziki wa kizazi kipya kutoka kwa wanamuziki wakali, Mwasiti Almasi, Maunda Zorro, Estelina Sanga ‘Linah’, Mzee Yusuf akiwa na kundi zima la Jahazi Modern Taarab bila kumsahau Juma Nature na TMK Wanaume Halisi.”
Kwa upande wa mabondia hao, kila mmoja ametamba kumchakaza na kumstaafisha mwenzake, wakati wanamuziki hao, wameahidi burudani ya kihistoria.
Kuhusu watoto, Mrisho alisema kuwa siku hiyo watapewa kipaumbele, kwani watapewa chakula kwa ajili ya kusherehekea sikukuu, vilevile wale watakaokuwa wanasherehekea siku ya kuzaliwa, watafanyiwa sherehe palepale.
(PICHA NA ERICK EVARIST / GPL).
Copyrights Tabitha Hudson 2012
0 comments:
Post a Comment