Ads 468x60px

Thursday, September 06, 2012

Wabunge waliotuhumiwa kwa rushwa wanaweza kufukuzwa



Wabunge wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini waliotuhumiwa kwa rushwa huenda wakakabiliwa na hatari ya kuvuliwa ubunge na kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.


Wabunge hao kutoka chama tawala na vyama vya upinzani wanaweza wakapoteza nyadhifa zao ikiwa Kamati ndogo Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayochunguza sakata hilo itathibitisha kama ni kweli walipewa rushwa.

Naibu Spika, Job Ndugai, alisema hayo juzi usiku wakati akizungumza katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha  ITV jijini Dar es Salaam.

Alisema Kamati ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo (CCM), Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan Ngwilizi, inao uwezo wa kupendekeza kama wabunge hao wavuliwe nyadhifa zao au washitakiwe mahakamani.

“Kamati ndogo ya Bunge iliyoundwa na Spika Anne Makinda, ikimaliza kazi yake na ikathibitisha kuwa ni kweli wapo wabunge waliopewa rushwa inaweza ikatoa mapendekezo ambayo yanaweza kupelekea mbunge akapoteza nafasi yake,” alisema Ndugai.

Ndugai alisema Kamati ya Bunge ni chombo muhimu sana ambacho kinachambua mambo kabla hayajapelekwa bungeni, hivyo inatakiwa kuwa makini.

Alisema kunapokuwa na kamati inayolegalega inaweza ikalipotosha Bunge na kwamba kutokana na hali hiyo ndiyo maana Spika Makinda alichukua uamuzi wa kuvunja Kamati ya Nishati na Madini kutokana na kuwapo kwa wajumbe kutoelewana, kutuhumiana na kuwa na mahusiano yasiyokuwa ya kiafya.

“Ndani ya wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini kulikuwa na mahusiano yasiyokuwa ya kiafya, baadhi walikuwa wanataka Waziri wa Nishati na Madini, Naibu Waziri na Katibu Mkuu waondolewe, hivyo isingekuwa rahisi wakafanya kazi pamoja,” alisema Ndugai.

Spika Makinda aliunda kamati hiyo Agosti 2, mwaka huu wakati wa Mkutano wa Nane wa Bunge. 

Wajumbe wake ni John Chiligati (Manyoni Magharibi-CCM); Riziki Omar Juma (Viti Maalum-CUF); Said Amour Arfi (Mpanda Mjini-Chadema) na Gosbert Blandes (Karagwe-CCM).

Kamati hiyo ilipewa wiki mbili na baadaye  kuongezewa muda zaidi hadi Septemba 15, mwaka huu kutokana na baadhi ya waliotakiwa kuhojiwa kuwa nje ya Bunge.

Aliunda kamati hiyo baada ya kuivunja Kamati ya Nishati na Madini kufuatia madai kuwa baadhi ya wajumbe wake walihongwa na kampuni za mafuta ili washinikize kuondolewa kwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Mhongo na Katibu Mkuu, Eliakim Maswi.

Maswi alituhumiwa kuipa zabuni Kampuni ya Puma Energy ya kuagiza mafuta mazito ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Wabunge kadhaa walizungumzia tuhuma za wenzao kuhongwa wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini iliyowasilishwa bungeni Julai 27, mwaka huu.

Kamati hiyo ilivunjwa kufuatia hoja ya Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa, kuomba mwongozo na kumtaka Spika kuivunja kamati hiyo kutokana na tuhuma za baadhi ya wajumbe wake kuhongwa.

Akizungumzua kuhusu mivutano ya wabunge inayotokea bungeni, alisema ni jambo la kawaida kwa sababu Bunge linawakutanisha wabunge kutoka vyama mbalimbali vya siasa.

Ndugai alisema Watanzania wanatakiwa kuwasifia viongozi wanaoliongoza Bunge kwani wanafanya kazi nzito kwani vyama vya siasa vikimaliza mikutano ya kwenye majukwaa ya vyama mbalimbali wakishamaliza mapambano kwenye mikutano yao, mahali pekee wanapokutana ni bungeni.

“Malumbano ni kitu ambacho kinatarajiwa bungeni, ni jambo la maendeleo wala siyo jambo baya. Tatizo kubwa ni pale ambapo baadhi ya wabunge wanasema uongo wa wazi kwa makusudi ili tu chama kingine ama serikali kionekane ni kibaya kwa jamii,” alisema Ndugai.

Ndugai alisema kilichosumbua sana katika Mkutano wa Nane ni matumizi ya lugha za kuudhi na kejeli.

“Mtu kama amekasirika aonyeshe kukasirika kwake siyo kutoa lugha chafu na ndiyo maana tunaitwa waheshimiwa, wabunge lazima turudi kwenye misingi ya kuwa wastaarabu miongoni mwetu hata unapozungumza dhidi ya chama fulani hata kama unapingana nao, lazima uzungumze katika lugha ambayo ni ya staha,” alisema Ndugai.

habari na THOBIAS MWANAKATWE
CHANZO: NIPASHE

Copyrights Tabitha Hudson 2012

0 comments: