Na: Florence Majani na Herieth Makwetta. Mwananchi
TATIZO la uzazi linaonekana kushika kasi nchini baada ya idadi kubwa ya wanandoa kukimbilia Kenya kupata huduma ya upandikizaji wa watoto kwa gharama ya zaidi ya Sh5 milioni.Kati ya wageni 10 wanaokwenda katika vituo vya upandikizaji vya Aga Khan na Nairobi IVF Centre nchini humo, wanne wanatoka Tanzania.
Licha ya kuwapo kwa huduma hiyo nchini, imeelezwa kwamba Watanzania wengi wanakimbilia huko kutokana na unafuu wa gharama na ubora wa huduma.
Huduma hiyo ni ya mwanamke kupandikizwa mbegu ya kiume ili kuweza kushika mimba na baadaye kupata mtoto.
Mmiliki wa Kituo cha Upandikizaji cha Nairobi (Nairobi IVF Centre), Dk Joshua Noreh alisema kwa mwaka kliniki yake hupokea zaidi ya wagonjwa 270 kutoka mataifa mbalimbali likiwamo Bara la Ulaya.
Alisema wagonjwa kutoka Tanzania walianza kumiminika katika kliniki hiyo kuanzia mwaka 2006 na ukiondoa gharama za matibabu ambazo ni Sh5.4 milioni zipo gharama za ushauri na uchunguzi wa tatizo.
“Gharama ya ushauri peke yake ni Sh42,000 za Tanzania. Baada ya ushauri, mgonjwa hutozwa Sh420,000 kwa ajili ya uchunguzi wa tatizo. Gharama za matibabu hutegemea ukubwa wa tatizo. Tiba yenyewe ni upandikizaji wa mbegu, hadi hatua za kuirutubisha,” alisema.
Dk Noreh alisema ukijumlisha gharama za usafiri, malazi, mlo na tiba kwa wagonjwa wanaotoka Tanzania, wengi wao hutumia kati ya Sh8milioni hadi Sh10 milioni, kwa ajili ya kupata mimba.
Imeelezwa kuwa raia wa Uganda hukimbilia Kenya kukwepa gharama kubwa kwani nchini humo hugharimu kiasi cha Sh500,000 ya Uganda (sawa na Sh9.5 milioni) wakati huduma hiyo hupatikana Kenya kwa Sh300,000 (sawa na Sh5.4 milioni) kwa mzunguko.
“Tuna vituo zaidi ya vitano vya IVF hapa Kenya, ndiyo maana Kenya imekuwa kimbilio la wanandoa au wapenzi kupata matibabu ya aina mbalimbali za ugumba. Lakini kikubwa ni huduma bora na gharama nafuu ndiyo sababu ya ongezeko hili la wageni kutoka nje.”
Alisema baadhi ya nchi hazina huduma ya IVF hivyo wanandoa huenda Kenya na wengine wanayo huduma hiyo katika nchi zao ila wanachagua Kenya kwa sababu ya urahisi wa tiba hiyo na kuwapo kwa mbegu za wanaume wa Kiafrika zilizohifadhiwa.
Nchi nyingine ambazo wanandoa wake wanaongoza kwenda Kenya kwa ajili ya kupata huduma ya upandikizaji wa watoto ni Uganda, Sudan ya Kusini, Marekani na Ethiopia.
Mtaalamu kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan Nairobi, Dk Prafull Patel alisema idadi ya wanaohitaji huduma hiyo imekuwa ikiongezeka kwa kasi kutoka mataifa ya Afrika, Uingereza na Marekani.
Alisema zaidi ya robo tatu ya wanaopata huduma hiyo ni watu kutoka nje ya Kenya, lakini hasa ni kutokana na unafuu wa gharama za huduma hiyo ikilinganishwa na nchi nyingine.
Nchini Uganda, IVF inagharimu Sh9,000,000 za Tanzania wakati Uingereza inagharimu zaidi ya Sh10,800,000 za Tanzania na kwa wenza zinafikia Sh21,600,000 kwa kila mzunguko huku Marekani ikigharimu Sh10,620,000 na Sh19,800,000 kwa mzunguko.
Hii inamaanisha kwamba gharama nchini Kenya ni nusu ya gharama inayolipiwa Marekani, Ulaya na nchi nyingine za Afrika. Hiyo inaelezwa kuwa chanzo cha ongezeko la idadi ya wageni kwenda Kenya kusaka tiba ya ugumba.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz
Copyrights Tabitha Hudson 2012
0 comments:
Post a Comment