Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi akiwaonyesha wadau waliohudhuria hafla fupi ya makabidhiano chupa ya dawa ya kutibu ugonjwa wa vikope aina ya Zithromax zilizotolewa na kampuni ya kimataifa inayofanya utafiti na utengenezaji wa Dawa ya PFIZER kutoka Marekani leo jijini Dar es salaam. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi akiangalia moja ya boksi la dawa za kutibu ugonjwa wa vikope aina ya Zithromax zilizotolewa na kampuni ya kimataifa inayofanya utafiti na utengenezaji wa Dawa ya PFIZER kutoka Marekani leo jijini Dar es salaam. Wengine ni Bi. Caroline Roan makamu wa Rais wa kampuni hiyo huduma za jamii (katikati) na Dkt. Peter Mbuji Kaimu Mkurugenzi Idara ya Kinga(kushoto). =========== ======== ======== ======= WILAYA 40 NCHINI KUPATIWA DAWA ZA KUTIBU UGONJWA WA VIKOPE . Na. Aron Msigwa –MAELEZO. 21/9/2012, Dar es salaam. Wilaya 40 nchini zitarajia kunufaika na mkakati wa kutokomeza ugonjwa wa Vikope kufuatia kampuni ya kimataifa inayofanya utafiti na utengenezaji wa Dawa ya PFIZER kutoka Marekani kupitia mpango wa kimataifa wa kupambana na Ugonjwa wa vikope kuipatia Tanzania msaada wa dawa aina ya Zithromax kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo. Akizungumza wakati wa makabidhiano ya dawa hizo leo jijini Dar es salaam ,Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekua ikifanya mikakati ya kudhibiti ugonjwa wa Vikope na kutoa elimu ya afya kwa jamii juu ya namna ya kupambana na ugonjwa huo. Amesema kuwa Wizara ya afya inaendelea kupambana na magonjwa yaliyosahauliwa ambayo yamekua yakiathiri watu kwa muda mrefu na kuongeza imekua ikisisitiza mbinu mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huo zikiwemo matumizi ya dawa, uboreshaji wa mazingira ,matumizi ya maji safi na salama pamoja na utoaji wa elimu. Ameongeza kuwa kampuni ya PFIZER kupitia mpango wa Kimataifa wa kupambana na Ugonjwa wa Vikope kwa mwaka 2012 imeipatia Tanzania msaada wa chupa 239,952 za dawa ya Zithromax zikiwa katika mfumo wa kimiminika na chupa za vidonge 17,520. “Ni matumaini yangu kuwa dawa hizi zitatoa msukumo wa kuondoa magonjwa haya kwa sababu tuna mkakati wa jumla wa kutokomeza na kuondoa kabisa ugonjwa huu na matokeo sasa ni mazuri” amesema. Kuhusu usalama na ubora wa dawa hizo Dkt. Mwinyi amesema kuwa dawa hizo zinakidhi viwango vya kimataifa na zina ubora na usalama kutokana na matumizi yake katika maeneo mbalimbali nchini toka mwaka 1999. “Nachosema sasa tiba tunayo, ubora na usalama wake ni wa uhakika wananchi msiwe na hofu yoyote kwa sababu dawa hizi hazina madhara” amesisitiza. Kwa upande wake makamu wa Rais wa upande wa mahusiano na huduma za jamii wa kampuni hiyo Bi. Caroline Roan amefafanua kuwa kampuni yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na magonjwa mbalimbali ikiwa ni sehemu ya mchango wake kwa jamii. Bi. Caroline amesema kuwa toka mwaka 1999 kampuni ya Pfizer imekuwa ikitoa msaada wa wa dawa za kukabiliana na ugonjwa wa Vikope/ Takoma kupitia mpango wa Kimataifa wa kupambana na ugonjwa huo (ITI). Kampuni ya Pfizer ambayo imekua ikitoa misaada ya dawa kwenye sekta ya afya nchini toka 1999 ina makao yake nchini Marekani ni miongoni mwa makampuni makubwa duniani yanayofanya kazi za utafiti, utengenezaji na usambazaji wa dawa katika nchi mbalimbali duniani ikiweka msukumo katika kuhakikisha kuwa binadamu mahali popote pale alipo anapata tiba sahihi na huduma bora za afya. |
Friday, September 21, 2012
WILAYA 40 NCHINI KUPATIWA DAWA ZA KUTIBU UGONJWA WA VIKOPE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment