MARANGU
KUFUATIA tukio la moto lililotokea katika hifadhi ya msitu wa mlima Kilimanjaro Julai saba mwaka huu kushika kasi katika maeneo ya Rombo na Kilema, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama ameziagiza Wilaya zote za mkoa huo, kutoa askari mgambo walioko katika wilaya zao kushiriki operesheni maalum ya kuzima moto huo.
Tayari watu zaidi ya 200 wakiwemo askari walioko kwenye mafunzo katika Chuo Cha Polisi Moshi wameendelea kushirikiana kuuzima moto huo ambao mpaka sasa wamefanikiwa kudhibitii moto huo kwa asilimia 75.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea neo hilo Meneja mahusiano kutoka hifadhi za Taifa (TANAPA) Pascal Shelutete alisema moto huo ulioanza siku ya jumapili julai saba umeendelea kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa bila kuathiri shughuli zozote za utalii katika hifadhi ya mlima.
Alisema moto huo ambao sasa unawaka katika maeneo mawili tofauti ikiwemo eneo la Rombo na Kilema juu imewalazimu kuweka kambi mbili tofauti ambapo kambi ya moja imewekwa eneo la Marangu kwa wanaozima msitu uliopo Kilema juu huku kambi nyingine ikiwa imewekwa Rombo kwa wale wanaozima maeneo ya Rombo.
Alisema moto huo umeathiri zaidi maeneo ya Amboni,Ushiri,Keryo,Kimori na Shimbi na kwamba kwa sasa jitihada zinafanyika kuhakikisha moto huo unakwisha na kwamba mpaka sasa taarifa za awali zinaonyesha chanzo cha moto huo ni watu waliokua wakirina asali kiholela waliwasha moto katikati ya m situ.
Alisema licha ya moto huo kuwa mkubwa na kuunguza zaidi ya hekari 40 haujaathiri shughuli zozote za kitalii zinazoendelea katika hifadhi ya mlima huo na kwamba shughuli zote za kitalii zinaendelea kama kawaida.
Alisema hifadhi ya Taifa kwa kushirikiana na jeshi la polisi wanaendelea na juhudi za kutafuta waliohusika na uharibifu huo na mara zoezi la kuuzima moto litakapokamilika taarifa ya tathmini ya madhara ya moto itafanywa.
Hii ni mara ya pili moto mkubwa kuwaka katika eneo hilo hilo ambapo moto kama huo uliwaka mwaka 2009 na kusababisha hasara kubwa kwa misitu na viumbe hai.